Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Majlisi hiyo ilifanyika katika mazingira yaliyojaa huzuni, tafakuri na mapenzi kwa Ahlul-Bayt (as), huku waumini wakisikiliza mawaidha, Qur'ani Tukufu, dua na kushiriki katika ibada mbalimbali za kuadhimisha siku hiyo yenye nafasi ya pekee katika historia ya Uislamu.
Sheikh Sajjad Amani, aliongoza jahazi katika kusimamia Majlisi hiyo, ambaye katika hotuba yake alielezea kwa kina falsafa ya mapinduzi ya Karbala na kusisitiza kuwa; Imam Hussein (as) alisimama kwa ajili ya kuilinda dini, kupambana na dhulma na kuhuisha maadili ya Kiislamu.
Sheikh Sajjad Amani aliwahimiza waumini kuendelea kushikamana na mafundisho ya Qur'ani Tukufu na Ahlul-Bayt (as), huku akibainisha kuwa ujumbe wa Ashura utaendelea kuwa chanzo cha mwamko wa kiroho, uadilifu na kupinga kila aina ya dhulma katika jamii.
Washiriki wa Majlisi walionesha hisia zao za majonzi kwa kusoma tenzi na nyimbo za maombolezo ya Imam Hussein (as), huku wakimuomba Mwenyezi Mungu awajaalie kuwa miongoni mwa wafuasi wa kweli wa njia ya Karbala na kuwathibitisha katika kusimama upande wa haki.
Maadhimisho hayo ni sehemu ya mwendelezo wa shughuli za waumini wa Ahlul-Bayt (as) duniani kote katika mwezi mtukufu wa Muharram, ambapo kumbukumbu ya tukio la Karbala huadhimishwa kwa lengo la kuhifadhi na kueneza ujumbe wa kujitolea, haki, uhuru na uadilifu uliodhihirishwa na Imam Hussein (as).





Maoni yako